Tanzania leo imejitutumua mbele ya Namibia baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa pili kundi D, michuano ya CHAN.
Bao la Farid Mussa aliloweka kambani kwenye dakika ya 65 liliihakikishia Tanzania ushindi muhimu ambao unaweka hai matumaini ya kufuzu hatua ya mtoano.
Tanzania ilitawala mchezo huo kwenye kipindi cha kwanza, wakitumia mipira mirefu ambayo ilikuwa ikiwapa changamoto walinzi wa Namibia.
Katika kipindi cha pili Namibia walirejea wakiwa bora zaidi lakini kazi nzuri iliyofanywa na Ayubu Lyanga, aliyepiga krosi maridhawa ambayo ilitua kichwani kwa Ditram Nchimbi aliyemtengea Farid kufunga bao hilo muhimu.
Kazi nzuri pia ilifanywa na mlinda mlango wa Tanzania Aishi Manula ambaye aliliweka lango la Stars salama wakati Namibia wakiweka presha kusaka bao la kusawazisha.
Tanzania sasa inahitaji kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya Guinea ili kuweza kutinga hatua ya robo fainali.
Katika mchezo wa mapema, Zambia na Guinea zilitoshana nguvu baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Guinea inaongoza kundi ikiwa na alama nne sawa na Zambia timu hizo zikitofautiana bao moja.
Tanzania inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama tatu wakati Namibia imeyaaga mashindano hayo baada ya kipigo cha leo.
Katika mchezo wa Namibia dhidi ya Tanzania, Farid Mussa aliondoka na tuzo ya nyota wa mchezo huo.

0 Comments